KARIBU
klabu zote kubwa za soka barani Ulaya zimeandaa hundi ya kuidhinisha
malipo ya mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuinasa saini ya kiungo wa Borussia Dortmund, Ilkay Gundogan, ili ziweze kuimarisha vikosi vyao.
Kila zinapozungumzwa tetesi za uhamisho wa
wachezaji barani humo, jina la Gundogan linakuja kwanza hasa
yanapozungumziwa majina ya wachezaji wa kiungo. Ni nani huyu jamaa?
Gundogan alizaliwa katika kitongoji cha
Gelsenkirchen Oktoba 24, 1990. Wazazi wake wana asili ya Uturuki na ni
wahamiaji tu nchini Ujerumani.
Hii inamfanya awe sawa na wachezaji wengi wa
Kijerumani wa sasa ambao wazazi wao ni Waturuki, lakini walihamia
Ujerumani. Wachezaji hao ni kama vile; Nuri Sahin, Mesut Ozil na
wengineo.
Soka la vijana alilianza katika timu ya watoto ya
SV Gelsenkirchen-Hessler 06 kabla hajaibukia Schalke 04. Lakini maisha
yake ya soka katika timu ya wakubwa yalianzia Klabu ya Vfl Bochum msimu
wa 2008/09.
Msimu uliofuata alijiunga na FC Nurnberg,
ilikuwa mwaka 2009. Katika mechi yake ya nne tu ya Ligi Kuu Ujerumani
‘Bundesliga’ iliyochezwa Septemba 19, 2009 alitoa pasi ya bao katika
pambano dhidi ya wakali, Bayern Munich.
Bao lake la kwanza la ligi hiyo alifunga dhidi ya wababe hao hao wa Munich katika pambano la marudiano Februari 20, 2010.
Dortmund yamtolea jicho, la kumnasa. Macho ya
maskauti wa Dortmund yalimwona Gundogan na Mei 5, 2011 walimnasa na
akasaini mkataba wa miaka mitano. Aliifungia timu hiyo bao la kwanza
katika pambano la ugenini dhidi ya Freiburg.
Machi
20, 2012, Gundogan alifunga bao dakika ya 120 dhidi ya SpVgg Greuther
Furth katika pambano la nusu fainali ya michuano ya DFB-Pokal na
kuipeleka timu yake fainali.
Katika msimu wa 2012–13, Gundogan alikuwa mmoja kati ya wachezaji muhimu ambao walicheza soka la aina yake na kuipeleka Dortmund katika pambano la fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich lililofanyika katika Uwanja wa Wembley.
Gundogan alishirikiana na wakali wengine wa Dortmund kama Robert Lewandowski, Neven Subotic, Sven Bender,
Marco Reus, Mario Gotze, Mats Hummels, Jakub Błaszczykowski, Lukasz
Piszczek na wengineo kutengeneza kikosi kikali kinachoogopwa Ulaya mpaka
sasa.
Gundogan alicheza vizuri zaidi katika mechi zote
mbili za nusu fainali ambazo walijikuta wakipambana na wababe wa
michuano hiyo, Real Madrid.
Afunga fainali dhidi ya Bayern
Katika siku ya fainali dhidi ya Bayern, Gundogan
alifunga bao la penalti dakika ya 69 na kusawazisha. Hii ilikuwa penalti
yake ya kwanza kupiga katika maisha ya soka Dortmund. Bayern ilishinda
mabao 2-1.
Julai 27, 2013, Gundogan alifunga bao wakati Dortmund ilipoizamisha Bayern Munich 4-2 katika mechi ya kufungua msimu huu wa Bundesliga.
Aitosa Uturuki, akipiga Ujerumani
Baada ya miaka mingi ya kuchezea timu za vijana za Ujerumani, Gundogan aliitwa kwa mara
ya kwanza katika kikosi cha wakubwa cha timu ya taifa ya Ujerumani,
Agosti 2011 katika pambano la kirafiki dhidi ya Brazil. Hata hivyo
hakucheza mechi hiyo.
Mechi yake ya kwanza alikipiga dhidi ya Ubelgiji
Oktoba 11, 2011 akiingia kipindi cha pili katika ushindi wa mabao 3-1 wa
Ujerumani kufuzu michuano ya Euro 2012.
Kabla ya hapo, Gundogan alikuwa amefuatwa na
Shirikisho la Soka la Uturuki, lakini mwenyewe aliamua kuichezea
Ujerumani, nchi aliyozaliwa. Gundogan anakiri kwamba huu ulikuwa uamuzi
mgumu zaidi aliowahi kuuchukua maishani. Mei 2012, alichaguliwa na Kocha
wa Ujerumani, Joachim Low, katika kikosi cha wachezaji 23 wa michuano
ya Euro. Alipewa jezi namba mbili. Machi
26, 2013 alifunga bao lake la kwanza kwa Ujerumani katika pambano la
kufuzu michuano ya Kombe la Dunia wakishinda mabao 4-1 dhidi ya
Kazakhstan. Mechi hiyo ilichezwa katika Uwanja wa Grundig jijini
Nuremberg.
Gundogan anasifika zaidi kwa kucheza soka la pasi
kama ilivyo kwa Xavi Hernandez wa Barcelona. Haishangazi kuona
akihusishwa kujiunga na Barcelona ambayo inaamini atakuwa mbadala halisi
wa mkongwe wao huyo ambaye umri wake umeanza kumtupa mkono.Gundogan pia ni fundi mwenye uwezo mkubwa wa kupiga chenga.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!