Headlines News :
USWAZI MAGAZINE
Home » » MAKUNDI HASIMU YAJIUNGA KWA PAMOJA KATIKA AWAMU YA KWANZA YA MARIDHIANO YA MKOA WA JUBBALAND

MAKUNDI HASIMU YAJIUNGA KWA PAMOJA KATIKA AWAMU YA KWANZA YA MARIDHIANO YA MKOA WA JUBBALAND

Written By Unknown on Saturday, 9 November 2013 | Saturday, November 09, 2013

Wajumbe wakihudhuria siku ya mwisho ya awamu ya kwanza Mkutano wa Maridhiano ya Jubbaland mjini Mogadishu siku ya tarehe 6 Novemba. [Abdi Moalim/Sabahi]
Matokeo ya awamu ya kwanza ya Mkutano wa Maridhiano ya Jubbaland uliofanyika Mogadishu wiki hii ulipongezwa sana kama mafanikio kwa serikali ya shirikisho la Somalia na mchakato wa uundaji wa shirikisho.
Zaidi ya wajumbe 200 wakiiwakilisha serikali ya shirikisho, Serikali ya Mpito ya Jubba (IJA) wakiongozwa na Ahmed Mohamed Islam Madobe, viongozi mahasimu wakiwemo Barre Adam Shire Hirale na Iftin Hassan Basto, na washirika wa kimataifa, ukiwemo Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM), walihudhuria mkutano huo wa tarehe 3 hadi 6 Novemba.
Katika hitimisho la kongamano hilo, wajumbe walitoa wito wa amani na umoja kwenye mkoa wa Jubbaland, na kukubaliana kumaliza uhasama miongoni mwa watu na kufanya kazi pamoja katika kusaidia mchakato wa uundaji wa shirikisho.
Wajumbe hao pia walijadili mchakato wa ujengaji wa amani, masuala ya usalama na maridhiano, namna ya kuviingiza vikundi vya ndani vyenye silaha kwenye Jeshi la Taifa la Somalia, na jinsi ya kuongeza mapambano dhidi ya al-Shabaab.

Makubaliano yazileta pamoja pande hasimu

Wajumbe 12 wakiwakilisha pande za kisiasa za mikoa ya Jubba la Gedo kwa pamoja walisaini azimio la mwisho la makubaliano.
Kati ya wajumbe hao 12, sita waliwakilisha serikali ya sasa ya mpito inayoongozwa na Madobe, ambapo wengine sita waliwakisha mahasimu wake katika kinyang'anyiro cha urais wa Jubbaland, akiwemo mjumbe mmoja aliyesaini makubaliano hayo kwa niaba ya Hirale.
Hirale anaongoza kundi la wanamgambo ambalo liko umbali wa kilomita 10 kutoka Kismayu na alikuwa hasimu mkubwa wa Madobe wakati IJA ilipoanzishwa. Hadi sasa hajamuunga mkono Madobe na amekuwa mkosoaji wa serikali ya shirikisho.
Abdi Shire Warsame, aliyesaini makubaliano hayo kwa niaba ya Hirale, alisema Hirale alifurahishwa na matokeo ya kongamano hilo, ingawa hakuweza kushiriki kwa sababu binafsi.
"Kwa upande wetu, tumedhamiria kutafuta amani kwa ajili ya watu wanaoishi huko, lakini ni muhimu kwa serikali ya sasa [ya Jubba] pia kubeba jukumu la suala hili," aliiambia Sabahi.
Alisema makubaliano hayo yanaweza kupelekea amani, lakini yanahitaji kutekelezwa kwa vitendo.
Hirale atahudhuria awamu ya pili ya kongamano hilo ambalo litafanyika Kismayu, alisema Warsame. Tarehe ya kongamano hilo la Kismayu bado haijapangwa.
Abdulqadir Haji Lugadhere, mmoja wa watu waliosaini makubaliano hayo akiwakilisha kambi ya Madobe, alisema IJA pia ilifurahishwa na makubaliano yaliyofikiwa kwenye duru hii ya mazungumzo.
Aliipongeza serikali ya shirikisho kwa jukumu lake katika kuongoza kile alichokiita kongamano "lenye manufaa" na kwa kuunga mkono IJA.
Lugadhere alisema serikali ya Madobe itahakikisha kwamba watu wote wa mikoa ya Gedo na Jubba wanajumuishwa kwenye utungaji sera. "Hakuna atakayetengwa, kila mmoja atakuwa sawa," aliiambia Sabahi.
Katika duru ijayo ya mazungumzo mjini Kismayu, alisema, wadau watajadiliana namna bora kabisa ya kutekeleza mambo yaliyokubaliwa Mogadishu.

Waziri Mkuu wa Somalia, Abdi Farah Shirdon, akihutubia wajumbe kwenye sherehe za ufunguzi wa  Mkutano wa Maridhiano ya Jubbaland mjini Mogadishu siku ya tarehe 3 Novemba. [PICHA YA AFP/AU-UN IST/TOBIN JONES]
Waziri Mkuu wa Somalia, Abdi Farah Shirdon, akihutubia wajumbe kwenye sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa Maridhiano ya Jubbaland mjini Mogadishu siku ya tarehe 3 Novemba

Kubadili nia

Abdirahman Santur Moalim, mmoja wa wazee wa Kismayu aliyehudhuria kongamano hilo, alisema mwanzoni alikuwa anapingana na utawala wa Madobe, lakini sasa anaunga mkono uongozi wake baada ya kongamano la Mogadishu.
"Serikali hii inaona hili ndilo suluhisho na imetushawishi kuunga mkono utawala huu," aliiambia Sabahi. "Hivyo ndivyo tulivyokuja kuunga mkono makubaliano na tutashirikiana na utawala huu."
Moalim aliwatolea wito watu waliokuwa wakiupinga utawala huo hadi sasa kuunga mkono makubaliano ya amani, kwani yanaonekana kuwa yatajumuisha wote.
"Tulipoteza miaka 23 kwenye vita. Si vizuri kupingana na makubaliano haya, basi na tuchaguweni amani," alisema.
Hata hivyo, bado kuna wanasiasa na wazee wa kimila wanaopinga makubaliano haya na wanasema ni ya kibaguzi.
Mohamed Sayid Adam, mkaazi wa Beled Hawo katika mkoa wa Gedo na mbunge wa zamani wakati wa Serikali ya Shirikisho ya Mpito, alisema kuwa makubaliano hayo yalikuwa mabaya na yanapotosha.
"Makubaliano [ambayo yalisainiwa] mjini Mogadishu sio suluhisho kwa mikoa ya Jubba na Gedo," aliiambia Sabahi. Adamu, aliishutumu serikali kwa kukanyaga sheria na kudharau mfumo sahihi wa kuunda serikali za shirikisho.
"Tulitaka maeneo yanayodhibitiwa na al-Shabaab katika mikoa hii kuwekwa huru kwanza, na baadaye watu wafanye maamuzi ya maisha yao ya baadaye. "Hili lazima liletwe katika makubaliano na katiba."
Hassan Hiloule Osman, mzee wa kimila kutoka ukoo wa Hawadle, aliiambia Sabahi kwamba ukoo wake haukualikwa katika mkutano na unahisi umetengwa.
"Sisi ni miongoni mwa watu wanaoishi katika Jubba na hatukushauriwa kuhusu mkutano huo," alisema.

Maslahi ya taifa juu ya maslahi kibinafsi

Wakati wa sherehe za ufungaji wa mkutano, Rais Hassan Sheikh Mohamud alitoa wito kwa watu wa mikoa ya Gedo na Jubba kuunga mkono makubaliano hayo, kwa kusema kwamba mwishowe wataongozwa utawala ambao unawakilisha jamii zote katika eneo hilo.
"Ni heshima kushiriki katika mkutano muhimu na wakihistoria kama huu unaohitaji dhamira yetu ya pamoja kwa kutuongoza katika maridhiano ya kudumu ili kudumisha amani ya kikanda na mafanikio," Mohamud alisema.
"Madhumuni ya mkutano huu ilikuwa kwa watu katika mikoa kuzungumzia masuala na kutatua mambo ya mikoa yao," alisema. "Ni muhimu sana kwa Uongozi wa Mpito wa Jubba kuwa ya kwanza inayowakilisha katika eneo hilo na kwamba watu wote wanashirikishwa katika sera. Kwa sababu hiyo, lazima [tuendelee mbele] kwa ukomavu, subira, uvumilivu na kuweka masilahi ya taifa mbele ya maslahi binafsi."
"Lengo letu la muda mrefu ni kuiongoza nchi hadi pahala ambapo inaweza kushindana na nchi nyengine duniani. Tunataka Somalia kuwa na uzito kimataifa, na hilo linaweza kufikiwa ikiwa tumeungana na kutafuta njia ya maridhiano endelevu," alisema.
Naye Waziri Mkuu Abdi Farah Shirdon aliyaita makubaliano hayo kuwa ni "mafanikio makubwa na fursa kubwa sana" kwa kanda hiyo.
"Makubaliano haya yanazipa jamii zote za Jubba fursa ya kusonga mbele kuelekea eneo lenye amani na lililoungana," alisema katika taarifa baada ya mkutano.
"Ninaitaka IJA kuwa jiwe la kupandia kufikia serikali ya shirikisho ya Jubbaland yenye mamlaka kamili na alama ya mafanikio ya shirikisho kwa Somalia," Shirdon alisema. "Makubaliano haya yanaipa Jubbaland na Somalia fursa hiyo."
Mwakilishi Maalumu wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika kwa Somalia Mahamat Saleh Annadif pia alisifia matokeo ya mkutano huo.
"Ninataka kuthibitisha utayari wa Umoja wa Afrika na hasa ule wa AMISOM katika kuusaidia utekelezaji wa mapendekezo yaliyofanywa wakati wa mkutano, alisema katika taarifa.

Tamko la mwisho

Baadhi ya waimbaji wakiimba wakati wa sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa Maridhiano ya Jubbaland mjini Mogadishu siku ya tarehe 3 Novemba. [PICHA YA AFP/AU-UN IST/TOBIN JONES]
Baadhi ya waimbaji wakiimba wakati wa sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa Maridhiano ya Jubbaland mjini Mogadishu siku ya tarehe 3 Novemba.
Kwa mujibu wa tamko lililotolewa baada ya kumalizika kwa mkutano huo, pande zinazohusika zilikubaliana:
• Kwamba pande zote zikubali Makubaliano ya Addis Ababa ya mwezi Agosti 2013.
• Kwamba watu wa Jubba wajitahidi kujenga makubaliano, kusameheana, kutatua masuala ya mali, kuepuka machocheo yanayoweza kusababisha migogoro.
• Kwamba wadau wote waunge mkono muundo jumuishi wa utawala wa mpito utakaokamilika kwa kuzingatia haki za watu wachache, na serikali ya shirikisho ya Somalia inapaswa kuchukua jukumu la uongozi katika suala hili.
• Kwamba awamu ya mwisho ya mkutano wa maridhiano ufanyike Kismayu.
• Kwamba jukumu la asasi za kiraia katika mikoa Jubba itaimarishwa.
Wajumbe hao pia walikubaliana kujenga na kuunganisha vikosi vya usalama Jubba ikiwa ni pamoja na polisi, wanajeshi na walinzi katika jeshi la umoja wa kitaifa. Pia walipendekeza kwamba fursa nyengine za ajira nyingine zitengenezwe kwa ajili ya wale ambao hawako tayari kujiunga na jeshi.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Share Na Jamaa Yako :

0 comments:

Toa Maoni yako

Tuambie Unafikilia Nini..!

Followers

Facebook Fan Page

Tukutane Twitter

Walio Tembelea Website Hii

Advertise

Smiley face
 
Support : Ismail Niyonkuru | Gody Godwin Unstoppable
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Ahabona 24 - Haki Zote Zimehifadhiwa
Template Design by Gody Godwin Unstoppable Published by Uswazi