STRAIKA wa Simba,kutoka hapa nchini Amissi Tambwe, ametamka kwamba Yanga
watasubiri sana kipindi hiki, kwani Wekundu wa Msimbazi sasa ni habari
nyingine kabisa. Kocha wake, Zdravko Logarusic, naye amekejeli akisema
Yanga hawamuwezi na ataendelea kucheza na akili zao ili kuwapa vipigo.
Simba iliifunga Yanga mabao 3-1 juzi Jumamosi kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na vyombo vya habari huku akicheka, Tambwe
alisema: “Aisee kwa muziki huu tulionao sasa, Yanga watasubiri sana kwa
sababu tumewazidi kila kitu, sisi ni wajanja. Mfano ni mechi ya
Jumamosi, si umeona mwenyewe maana kila idara tuliwazidi, huwa wanatamba
na mabeki wao wale, Yondani (Kelvin) na Cannavaro (Nadir Haroub) na
siku ile tuliwapoteza kabisa.
“Ili uamini kwamba ilikuwa mechi mbaya kwao, ni
ile kadi nyekundu aliyoonyeshwa Yondani. Katika mechi yoyote, ukiona
mchezaji anapata kadi nyekundu ujue ni dalili tosha ya timu yake
kuzidiwa, niliingia nikijiamini na niliamini naweza kufanya vile kama
matokeo yalivyopatikana.
“Kasi yangu ndivyo itakavyokuwa kwa sababu nacheza na wachezaji ambao nao wanajua mpira vizuri, lakini kocha naye ni mzuri.”
Tambwe ambaye alifunga mara mbili katika mechi hiyo, pia ndiye kinara wa mabao kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara. Ana mabao 10.
Kocha wa Simba, Logarusic, ambaye muda wowote
anatarajia kwenda kwao Croatia kwa mapumziko ya sikuku za Noeli na Mwaka
Mpya, alisema: “Unajua tuliingia uwanjani lakini sehemu kubwa ya
matumaini ya mashabiki walijua Yanga ndiyo itashinda na hata Yanga
wenyewe walijua wanashinda.
“Nilichokifanya ni kucheza na akili zao
nikawajenga wachezaji wangu kisaikolojia na kuwapa maelekezo, wachezaji
nao walinielewa na tukafanikiwa. Niliwaambia wajiamini na wakinisikiliza
mimi tutashinda, ndiyo ikawa vile.
“Pia mazoezi yalisaidia kwa kipindi chote
tulichokuwa kambini, ndiyo siri kubwa ya mafanikio yetu, wachezaji ni
wasikivu sana na walijua lazima tushinde kwa vile tumebezwa sana.”
Katika mchezo huo, Simba ndiyo ilitawala kwa kiasi
kikubwa katika safu zote kuanzia beki iliyokuwa chini ya Joseph Owino
raia wa Uganda, Mkenya Donald Musoti, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Haruna
Shamte, wakati Jonas Mkude, Henry Joseph walicheza kiungo, Awadh Juma,
Haruna Chanongo walicheza winga na washambuliaji wa kati walikuwa, Said
Ndemla alicheza namba 10 na Tambwe.
Logarusic ambaye huwa hataki utani na kazi,
alikuwa akimtoa kila mchezaji aliyeona analeta masihara au amezidiwa na
alifanya hivyo kwa Ndemla, Henry, Awadh, Chanongo na Tambwe na
kuwaingiza, Zahoro Pazi, Amri Kiemba, Ramadhani Singano ‘Messi’,
Ramadhani Chombo Redondo ambaye naye hakuchukua muda nafasi yake
ilichukuliwa na Abdulhalim Humoud.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!