WAASI WA SUDAN KUSINI WAONYWA TENA VIKALI NA SERIKALI
Waziri wa Habari nchini Sudan Kusini ametangaza kuwa, ikiwa waasi
hawatatekeleza mapendekezo yaliyotolewa na serikali ya Juba kwa ajili ya
kusitisha mapigano, basi vikosi vya serikali hiyo vitaanzisha
mashambulizi makali dhidi ya maeneo muhimu yanayodhibitiwa na waungaji
mkono wa makamu wa zamani wa rais Bwana Riek Machar. Michael Makuei
amesema kuwa, vikosi vya serikali pia vimefanikiwa kuwafurusha waasi
katika mji wa Mayom katika jimbo la al-Wahda nchini humo. Ameongeza
kuwa, ikiwa Riek Machar hatokubali kukomesha machafuko, basi vikosi vya
nchi hiyo havitakuwa na budi ispokuwa kumfurusha kiongozi huyo wa waasi
kutoka katika mji wa Bentiu. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, mji wa
Bentiu ndio makao makuu ya mwisho yanayodhibitiwa na askari wanaomuunga
mkono Riek Machar aliyekuwa makamu wa rais wa Salava Kiir. Kwa upande
mwingine Makuei amesisitiza kuwa, kazi ya usitishaji mapigano imebakia
mikononi mwa kiongozi huyo wa waasi na kwamba serikali ya Sudan Kusini
imeshafanya juhudi nyingi kwa ajili ya kuhakikisha jambo hilo
linafikiwa. Hii ni katika hali ambayo Ijumaa iliyopita, serikali ya Juba
ilitoa mapendekezo ya kusitisha mapigano sambamba na kuahidi
kuwaachilia huru wanasiasa wanane kati ya 11 ambao wanashikiliwa na
serikali ya Juba na vinara wa upinzani wa serikali na waungaji mkono
wakubwa kwa Bwana Riek Machar.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!