MAMIA ya wasafiri walikwama barabarani na
wengine walilazimika kugharamia zaidi usafiri Alhamisi asubuhi baada ya
lori la mafuta kuanguka katika eneo la General Motors (GM) na kufunga
njia kwa watu wengi wanaotumia barabara ya Mombasa kuelelekea maeneo ya
katikati mwa jiji na kwingineko.
Watu
waliokuwa wakielekea maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo
Kenyatta, Kitengela na Machakos pia waliathiriwa baada ya barabara hiyo
kuanza pia kutumiwa na magari yaliyokuwa yakielekea jijini.
Hata hivyo, lori hilo lilifanikiwa kuondolewa barabarani baada ya zaidi ya masaa matano tangu lilipoanguka.
“Lori
lilianguka mwendo wa saa kumi usiku likiwa na mafuta ghafi ya kutengezea
mafuta ya kupikia.Dereva aliumia na kupelekwa hospitalini. Gari hilo
lilionekana kupoteza mwelekeo,” Kamanda wa Trafiki Samuel Kimaro alisema.
Aliongeza,
“Ilituchukua masaa mengi kuondoa trela hilo kwa kuwa lilikuwa na uzito
mkubwa. Kila kreni iliyokuja ilikuwa inashindwa. Na hatimaye
tulipoindoa, tulikumbana na tatizo lingine la mafuta yaliyokuwa
yamemwagika na kufanya barabara kuteleza mno. Tulijitahidi kusafisha
barabara na sasa hali ni shwari, shughuli zinaendelea kama kawaida.”
Matatu nyingi
zilitumia msongamano huo kuongeza nauli, baadhi zikitoza Sh150 na Sh200
kutoka Mlolongo kuelekea jijini ilhali kawaida safari hiyo huwa kuanzia
Sh40 hadi Sh80.Nyingine ziliamua kufanya safari fupi na kuwafikisha
abiria mahali msongamano wa magari ulionekana kufika.
Idadi kubwa ya watu ilionekana kutamaushwa na nauli hiyo na walionekana wakiwa wamesimama kwenye steji mbali mbali.
Hata hivyo,
abiria wengi pia walionekana kushuka kutoka magari hayo hata baada ya
kulipa na kuamua kutembea baada ya kusubiri kwa muda wa zaidi ya saa
moja bila magari hayo kusongea.
Gari moshi la
Syokimau pia lilishuhudia msongamano mkubwa wa watu katika treni zake
mbili za saa moja na saa tatu, baada ya watu wengi kuamua kuliabiri ili
kukabiliana na msongamano huo.
Bi Ann
Muteti, alisimulia kusubiri steji kwa muda mrefu kuanzia saa moja bila
kupata gari kabla ya kuamua kuelekea kwa kituo cha reli cha Syokimau,
kusafiri na treni ya saa tatu.
Nao wahudumu
wa bodaboda walifanya biashara kubwa wakisafirisha abiria ambao walihisi
kuchelewa kazini ama waliokuwa wakielekea kwa sehemu za karibu kama
Cabanas na GM.Wengine wanaofanya kazi katika maeneo ya karibu kama
Cabanas ambapo kawaida wao hutozwa Sh20 kutoka Mlololongo na Syokimau,
waliamua kutembea ili wasichelewe kazini.
Msongamano
huo pia ulifanya Halmashauri ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA) kutoa
tahadhari kupitia kwa mtandao wa twitter kwa wenye safari za ndege
kuanza kuelekea huko mapema.
Tukio hilo
pia lilisababisha msongamano kwenye barabara nyingine baada ya wenye
magari kujaribu kuhepa Mombasa Road, na kutumia ya Outering, Jogoo na
Enterprise.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!