Siku kama ya leo miaka 35
iliyopita, inayosadifiana na tarehe Pili Bahman 1357 Hijria Shamsia,
watu kadhaa waliuawa na kujeruhiwa, baada ya kujitokeza mapigano ya
barabarani kati ya wananchi wa Iran na vikosi vya utawala wa Kifalme nchini humo. Wananchi Waislamu wa Iran walikuwa kwenye maandalizi ya
kumpokea Imam Khomeini MA. Wananchi wa matabaka mbalimbali kutoka mijini
na vijijini walikuja mjini Tehran kwa shabaha ya kumlaki Imam Khomeini
MA akitokea uhamishoni nchini Ufaransa. Wakati harakati hiyo ya wananchi
ikiendelea, maafisa wasiopungua elfu nne wa jeshi la anga, walionyesha
uungaji mkono wao kwa wananchi, na kutangaza mgomo wa kula chakula,
sanjari na kutaka kufukuzwa washauri wa Kimarekani waliokuwepo nchini humo.
Tarehe 22 Januari miaka 453
iliyopita alizaliwa mwanafalsafa na mtaalamu wa hesabati wa Uingereza
Francis Bacon. Awali Bacon alijishughulisha na masuala ya kisiasa na
baadaye alifungwa jela kwa tuhuma ya kula rushwa.
Kipindi cha kufungwa jela
kilikuwa fursa mwafaka kwa Francis Bacon kudhihirisha kipawa chake.
Mwanafalsafa huyo alitoa mchango mkubwa katika kueneza Sayansi jarabati
nchini Uingereza na kuhuisha sayansi na falsafa barani Ulaya. Bacon
ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha New Atlantis.
Na miaka 985 iliyopita
alifariki dunia Abu Tayyib Tabari, faqihi na mwandishi wa Kiislamu huko
Baghdad. Abu Tayyib alizaliwa mwaka 348 Hijria huko Amul, moja kati ya
miji ya kaskazini mwa Iran. Tabari alifanya safari katika nchi
mbalimbali kwa lengo la kutafuta elimu. Abu Tayyib Tabari aliishi na
kufundisha huko Baghdad ambapo alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa za
zama zake hizo. Faqihi Tabari alikuwa hodari katika taaluma ya fasihi na
utunzi wa mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu aliandika vitabu
mbalimbali na moja kati ya hivyo ni vile alivyoviita "Jawab fi Sama'a"
na "al Ghinaa wa Al Taaliqatil Kubra fil Furu'u".
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!