LICHA ya umilionea wake mkubwa unaoongezeka kila kukicha
kutokana na mafanikio yake makubwa katika soka, wazazi wa staa wa Real
Madrid, Gareth Bale wameendelea kuishi katika nyumba yao ya kimaskini
jijini Cardiff.
Si kwa sababu ya tabia za uchoyo za staa huyo,
hapana, Bale si mchoyo, lakini wazazi wake wenyewe wamemkatalia kuhamia
katika nyumba ya kifahari aliyowanunulia kwa sababu wanapenda kuendelea
kukaa katika nyumba ya kota.
Bale, ambaye ni mwanasoka ghali zaidi duniani
baada ya kuhamishwa kwa kiasi cha Pauni 85 milioni kutoka Tottenham
Hotspur kwenda Real Madrid katika usajili wa kipindi cha majira ya joto
cha mwaka jana alisema angewapatia wazazi wake, Frank na Debbie kiasi
cha Pauni 1 milioni kwa ajili ya kutafuta jumba la kifahari la kununua
na kutimiza ndoto zao za kuishi maisha mazuri.
Lakini wazazi hao walimwambia Bale (24), kwamba
wamezoea na kusikia raha kuishi katika nyumba yao ya vyumba vitatu
ambayo Bale alikulia kabla ya kuibuka kuwa mchezaji ghali duniani.
Debbie (50), alimwambia rafiki wa familia yake
hiyo kwamba kitendo cha Gareth kuwapa ofa ya nyumba kilikuwa cha huruma
na kizuri, lakini wanapenda kuendelea kuishi walipo huku wakiwa na
majirani wazuri waliowazoea.
Yeye na mumewe, Frank (54), ambaye ni mstaafu wa
shule moja jijini humo, walinunua nyumba hiyo ya kawaida kwa kiasi cha
Pauni 12,000 miaka 30 iliyopita kabla ya Bale hajazaliwa na kwa sasa
nyumbani hiyo ina thamani ya Pauni 170,000.
Ni hapo ndipo walipomlea Bale na dada yake, Vicky
huku Bale akijifunza kucheza soka katika bustani iliyopo kando ya nyumba
hiyo na kuharibu mali za watu.
Baada ya kupatiwa kiasi hicho cha pesa na Bale kwa
ajili ya kusaka nyumba, yeye na mumewe walienda kutafuta nyumba ya
kifahari katika eneo la Vale of Glamorgan. Vile vile walitafuta nyumba
yenye thamani ya Pauni 415,000 karibu na eneo la wanaloishi.
Hata hivyo, mwishowe waliamua moja kwa moja kubaki
katika nyumba yao waliyoishi kwa miaka 30 iliyopita ambayo inaashiria
historia yao huku wakigoma kuwaacha majirani zao wenye upendo wa dhati
kwao.
Debbie alimwambia rafiki yake mmoja kuwa wanapata
kila wanachokitaka kwa kuwa hapo na itakuwa jambo gumu kwao kuhama
katika nyumba ambayo watoto wao walikulia.
Jirani yao, Bill Tout anasema kwamba amefurahi kwa
majirani zake hao kuamua kubakia katika nyumba hiyo kwa sababu ni watu
wema na wamezoeana kwa muda mrefu.
“Frank na Debbie ni watu wazuri sana na ni majirani bora. Mambo
hayatakuwa mazuri kama wakiamua kuondoka zao,” alisema Tout, ambaye ni
mjane mwenye umri wa miaka 82.
Bale bado ana upendo mkubwa kwa wazazi wake na
Septemba mwaka jana walikuwa katika Uwanja wa Santiago Bernabeu wakati
mtoto wao akitambulishwa kwa mashabiki wa timu hiyo huku akikabidhiwa
jezi namba 11 na Rais wa Real Madrid, Florentino Perez. Hata hivyo, Bale
mwenyewe anaishi katika jumba la kifahari lenye thamani ya Pauni 6.5
milioni ambalo analipia Pauni 10,000 kwa mwezi huku majirani zake wakiwa
ni pamoja na staa wa timu yake, Cristiano Ronaldo na mwigizaji maarufu
wa kike wa Hollywood, Penelope Cruz.
Winga huyo anayeingiza kiasi cha Pauni 300,000 kwa
wiki anaishi pamoja na mpenzi wake wa muda mrefu, Emma Rhys-Jones na
mtoto wao mwenye umri wa miezi 15.
Mara kadhaa Bale amekuwa akionekana katika vitongoji vya Cardiff akiwa anawatembelea wazazi wake na pia rafiki zake wa utotoni.
Inadaiwa pia kuwa Debbie na Frank waliingiza kiasi
cha Pauni 2 milioni katika uhamisho wa staa huyo wa Wales ambapo wote
wawili pamoja na mtoto wao, Gareth ni Wakurugenzi wa kampuni yao binafsi
waliyoianzisha, Primesure Limited ambayo ilinufaika na uhamisho huo.
Mtu mmoja wa karibu alinukuliwa na gazeti la The Mirror la Uingereza
akisema kwamba pesa hizo ni kama zawadi kutoka kwa Bale ambaye alitunzwa
vilivyo na wazazi hao mpaka kuibuka kuwa mmoja kati ya wachezaji mahiri
duniani.
“Gareth hajasahau alikotoka. Ni kijana mwaminifu.
Kipaumbele chake ni familia yake na tangu awe mchezaji mahiri wa kulipwa
amehakikisha wanapata kila kitu. Gareth anashukuru kwa kila
alichofanyiwa na wazazi wake wakati akiwa mchezaji chipukizi.”
“Mama yake Debbie alikuwa na hamu kubwa kuona dili
ya kwenda Hispania inafanikiwa kwa sababu yeye na Frank walikuwa sehemu
ya dili hilo.”
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!