HATUTAKI, na tena hatutaki hata kusikia.
Na ikiwezekana msirudi tena. Ndivyo ambavyo mapovu yamewatoka mdomoni
watu wa Manchester United baada ya PSG kurudi mezani juzi Jumapili na
ofa ya kumtaka kinda wao mahiri, Adnan Januzaj.
PSG wamekuwa wakitokwa udenda kwa kinda huyo
mwenye asili ya Albania aliyezaliwa Ubelgiji miaka 18 iliyopita na
hawajali kama aliingia mkataba mpya wa kuichezea Man United mwishoni mwa
msimu uliopita.
Hata hivyo, kocha David Moyes amekataa ofa hiyo ya
PSG inayodhaniwa kuanzia Pauni 25 milioni na kuendelea huku
wakisisitiza kwamba hawana mpango hata wa kukaa chini na kuzungumza na
matajiri hao wa mafuta kutoka Paris.
Man United imempatia mkataba mrefu wa miaka mitano
Januzaj Oktoba mwaka jana baada ya kugundulika kuwa huenda mchezaji
huyo angekuwa huru na kuondoka Mei mwaka huu mara baada ya msimu
kumalizika.
Kabla na baada ya kusaini mkataba huo, Januzaj
ameibuka kuwa miongoni mwa wachezaji wachache mahiri katika kikosi cha
Man United ambacho msimu huu kimekuwa kikisuasua ndani ya uwanja.
Kwa mujibu wa gazeti la Guardian la Uingereza, Januzaj angeingiza kiasi kikubwa cha pesa kama angeamua kukubali kwenda PSG, lakini mwenyewe ameamua kubaki Man United licha ya timu hiyo kuwa katika hatari ya kukosa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Katika mkataba wake wa awali nyota huyo alikuwa
akiingiza kiasi cha Pauni 1,000 tu kwa wiki kutokana na kuwa kinda
mwanafunzi, lakini mkataba wake wa sasa unamwingizia kiasi cha Pauni
30,000 kwa wiki.
Akiwa na PSG angeweza kuingiza kiasi cha zaidi ya
Pauni 80,000 kwa wiki, lakini staa huyo ameamua kubaki Man United na
kuendelea kujifunza zaidi wakati huu kocha Moyes akimwamini na kumpanga
mara nyingi zaidi katika safu ya ushambuliaji.
Wakati huohuo pia, PSG pia imekataliwa katika ofa
yao ya Pauni 14 milioni kwa ajili ya kumchukua kiungo mahiri wa
Newcastle United, Yohan Cabaye ambaye amekuwa akisakwa kwa muda mrefu na
kocha Laurent Blanc.
Newcastle inaamini kuwa staa huyo Mfaransa ana
thamani ya Pauni 25 milioni na inadaiwa kuwa hata Man United wameanza
kumtolea macho Cabaye.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!