JUAN Mata amesema ametua Manchester United kwa kazi moja tu;
kunyakua taji la Ligi Kuu England. Kabla hajamaliza, akamwambia kocha
David Moyes kwamba awe huru kumpanga popote pale ilimradi tu iwe kwenye
goli la wapinzani.
Anasema: “Nilikuwa nacheza kushoto nilipojiunga
Chelsea, msimu huu nilichezeshwa kulia na msimu uliopita, ambao ulikuwa
bora kabisa katika maisha ya soka langu, nilicheza nyuma ya mshambuliaji
wa kati. Lakini, mi sijali kitu, ilimradi niweke tu uwanjani nicheze
utaona mambo yangu.”
Akizungumza kwa mara ya kwanza akiwa mchezaji wa
Manchester United, kiungo huyo Mhispaniola anasema aliposikia David
Moyes anamtaka ajiunge Manchester United, kwanza alishusha pumzi na
kisha kuona hiyo ni nafasi yake ya kwenda kubeba ubingwa wa Ligi Kuu
England.
Mata anasema alipopata taarifa hizo akaanza
kuchati na Mhispaniola mwenzake, David de Gea, ambaye ni kipa wa miamba
hiyo ya Old Trafford.
Anasema: “David de Gea alinitumia meseji siku
chache zilizopita na kusema, ‘unakuja lini, utatua lini?’” kabla
hajanitania kwa kusema “unakuja kwa helikopta au kwa baiskeli?”.
Staa huyo ambaye ametua Old Trafford kwa pauni
37.1 milioni, amesema hatishwi na dau kubwa alilohamishiwa na kwamba
atakachofanya yeye ni kuonyesha vitu uwanjani.
Mata anatazamiwa kucheza mechi yake ya kwanza
Manchester United leo Jumanne usiku wakati klabu hiyo itakapomenyana na
Cardiff City kwenye Ligi Kuu England.
“Nafahamu dau nililohamishiwa ni kubwa, lakini mimi najiamini na nina uhakika mkubwa nitafanya vizuri,” anasema.
“Nitajaribu na siku zote ndivyo nilivyo. Kikosi
pamoja na kocha wote wazuri na mashabiki wa timu hii ni wa kipekee sana.
Hakika tuna kila kitu cha kutufanya tufanikiwe. Niliposikia Manchester
United inanitaka, nikasema ‘Wow’. Hii ni timu iliyotwaa mataji mengi na
yenye historia kubwa kwenye Ligi Kuu England na soka la nchi hii kwa
jumla. Ni heshima kubwa kwa klabu kama Manchester United kuona
inakutaka. Najisikia vizuri sana.”
Juzi Jumapili, uwanjani Stamford Bridge mashabiki
wa Chelsea walibeba mabango kumshukuru staa huyo kwamba wataendelea
kumkumbuka na wamempa asante kwa huduma ya nguvu aliyowapatia kwa
kipindi chote alichokuwa kwenye klabu hiyo.
“Nipo hapa Manchester United kwa sasa na nina
furaha kwa jambo hilo, nimekutana na David ni rafiki yangu mzuri sana na
hakuna ubishi jamaa ni kipa wa ukweli. Yeye amechangia sana mimi kuja
hapa,” anasema Mata.“Lakini, kwa mchezaji ambaye unapenda kufunga mabao, kutengeneza na
kuonyesha ufundi huwezi kugoma kwenda kwenye timu utakayocheza pamoja na
Wayne Rooney, Robin van Persie, Adnan (Januzaj), (Antonio) Valencia,
Chicharito (Javier Hernandez) na (Danny) Welbeck. Hawa ni wachezaji wa
viwango vikubwa na nitakachojaribu ni kuonyesha uwezo wangu kwa ajili ya
kusaidia timu.”
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!