AMECHOSHWA. Ni hivyo baada ya shabiki mmoja wa Manchester United
aliyeripotiwa alikuwa amelewa kuamua kupiga simu polisi na kuomba
apatiwe namba ya simu ya kocha wa zamani wa kikosi hicho, Sir Alex
Ferguson ili ampe yake ya moyoni.
Polisi wa Greater Manchester wamedai kwamba
walipokea simu ya shabiki huyo kupitia kwenye namba ya dharura ya 999
akiomba apatiwe namba ya Ferguson azungumze naye baada ya Man United
kutupwa nje na Sunderland kwa mikwaju ya penalti katika mechi ya nusu
fainali ya Kombe la Ligi Jumatano iliyopita.
Jambo hilo liliwafanya polisi hao kuwakumbusha
kwamba namba 999 ni kwa ajili ya huduma ya dharura tu na si kwa matumizi
mengine kama yaliyofanywa na shabiki huyo, aliyedaiwa kuwa alikuwa
amelewa. “Jana usiku (Jumatano iliyopita), saa 4.30 usiku saa za hapa
mtu mmoja kutoka Crumpsall alipiga simu kwenye namba 999 alikuwa kwenye
hali ya ulevi na kuomba azungumze na Sir Alex Ferguson baada ya matokeo
ya mechi,” ilibainisha taarifa hiyo ya polisi iliyowekwa kwenye ukurasa
wao wa Facebook.
“Sawa, ni hali ya kawaida kwa shabiki hasa timu
yako inapopoteza mchezo, lakini tunataka kuwakumbusha namba 999 ni ya
dharura. Kwa mahitaji mengine ambayo si ya dharura, namba inayoruhusiwa
ni 101.”
Polisi hao waliwapa ushauri mashabiki wa Man
United wakitaka kuzungumza na Ferguson basi wanapaswa kupiga simu moja
kwa moja kwenye klabu hiyo na si polisi.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!