Katibu Mkuu wa Zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan
amewasili Tehran kwa lengo la kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za
juu wa Iran kuhusu masuala kadhaa ya kieneo.
Annan ambaye ni mwenyekiti wa Taasisi ya Jopo la Wazee
aliwasili Tehran Alfajiri ya leo Jumapili akiwa ameandamana na rais wa
zamani wa Finland Aartti Ahtisaari ambaye pia ni mwanachama wa jopo hilo
. Wanachama wengine wa Jopo la Wazee ni Kasisi Desmond Tutu wa Afrika
Kusini na rais wa zamani wa Mexico Ernesto Zedillo na wanatazamiwa pia
kuwasili Tehran baadaye. Annan amenukuliwa akisema lengo la safari ya
siku tatu ya jopo hilo Iran ni 'kuhimiza na kuboresha roho ya uwazi na
mazungumzo baina ya Iran na jamii ya kimataifa sambamba na kutafuta njia
muafaka za kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kieneo.' Aidha
amesema 'Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu katika kudhamini
uthabiti Mashariki ya Kati.' Taarifa katika tovuti ya jopo hilo inasema
kutafanyika mazungumzo na maafisa wa Iran kuhusu njia za amani za
kusuluhisha migogoro na uhasama wa kimadhehebu Mashariki ya Kati. Jopo
la Wazee ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyoundwa mwaka 2007 kufuatia
pendekezo la rais wa zamani wa Afrika Kusini hayati Nelson Mandela.
Wanachama wa jopo hilo ni watu ambao wamewahi kushika nafasi muhimu za
uongozi katika nchi mbali mbali duniani.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!