Siku moja baada ya kushindwa kupata point tatu muhimu katika uwanja wa ugenini,meneja wa klabu ya Liverpool Brendan Rodgers amemkingia kifua beki kutoka nyumbani Afrika katika nchi ya Ivory Coast Habib Kolo Toure kufuatia kosa alilolifanya wakati wa mchezo dhidi ya West Bromwich Albion huko The Hawthorns.
Rodgers amesema anaamini Habib Kolo Toure alikuwa na malengo mazuri ya kuucheza mpira ambao walipewa pasi na mlinda mlango wa Liverpool Simon Mignolet, lakini kwa bahati mbaya alipokuwa kwenye harakati za kumpasia mchezaji mwingine wa The Reds mpira ulinaswa na Victor Anichebe na kuwafanya wenyeji kusawazisha.
Rodgers amesema katika soka makosa kama hayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara,hivyo amewataka mashabiki wa Liverpool kumsamehe Kolo Toure na kumuelewa kwamba hakukusudia kufanya kosa hilo bali ilikuwa ni bahati mbaya.
Amesema ataendelea kumuheshimu beki huyo mwenye umri wa miaka 32 na katu hatomvunjia heshima, kutokana na kumuamini na kuuthamini mchango wake tangu alipomsajili mwishoni mwa msimu uliopita akitokea Man City.
Katika hatua nyingine meneja huyo wa klabu ya Liverpool amesema kwa hakika kikosi chake kilionyesha mchezo mzuri wakati wote na hana budi kuyapokea matokeo ya sare ya bao moja kwa moja waliyoyapata.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!