KWELI pesa si kila kitu. Haiwezi kununua mapenzi. Aliyekuwa
mchumba wake anamiliki pato la Dola 20.5 milioni, lakini hilo halikuwa
na maana kwa mrembo wa Kibrazili, Bruna Marquezine, ambaye kipato chake
kizidishwe mara 30 ndiyo afikie kiwango cha mwanamume huyo.
Mrembo Bruna hakutazama nyuma na kuamua kumpa kisogo mwanasoka Neymar, ambaye pia ni Mbrazili mwenzake.
Kwa pesa anazopiga staa huyo wa Barcelona, wengi
waliamini isingekuwa rahisi kwa mrembo Bruna kuacha kuitumia nafasi hiyo
ya kuponda raha, lakini haikuwa hivyo. Sasa binti huyo amechukua njia
zake na kuamini kwa nguvu zake atapiga pesa za kutosha, hivyo hana haja
ya kumtegemea mtu.
Bruna Marguezini, ambaye jina lake la awali ni
Bruna Maia Reis, alizaliwa Agosti 4, 1995 mjini Duque De Caxias, Brazil.
Anatajwa kuwa na kipato cha Dola 700,000.
Kazi yake kubwa ni uigizaji na kutamba kwenye sinema mbalimbali nchini Brazil kumemfanya kuingiza kipato hicho. Kitu kilichompa sifa kubwa na kumpatia dili mbalimbali za kucheza sinema ni uzuri wake. Bruna anatajwa kuwa mwigizaji mrembo zaidi nchini Brazil.
Filamu yake ya kwanza ilikuwa Gente Inocente,
ambayo ilimpa umaarufu mkubwa na kumfanya awe na pesa. Pia binti huyo
ameng’ara kwenye vipindi mbalimbali vya televisheni zikiwamo tamthilia.
Bruna pia amekuwa akishiriki masuala ya mitindo na
mashindano ya kudansi kwenye televisheni ambayo yanamwongezea kipato.
Umahiri wake kwenye filamu umemfanya kushinda tuzo 11 kuanzia mwaka
2003.
Bruna alianza kuigiza akiwa na umri mdogo na
alionekana kwenye matangazo mbalimbali ya biashara na video za muziki.
Alipofikisha umri wa miaka minane alipiga hatua muhimu baada ya
kuonekana kwenye kipindi mashuhuri cha televisheni nchini Brazil
kilichokuwa kikiongozwa na Xuxa.
Baada ya kufanya vizuri hapo, mvuto wake ulimfanya
apate dili za kucheza tamthilia na televisheni yake ya kwanza kutamba
nayo ilikuwa ‘Rede Globo’. Baada ya hapo akaendelea kutesa kwenye
‘America’, ‘Cobras e Lagartos’, ‘Deseo Prohibido’ na ‘Negocios en China
Araguaia’.
Filamu alizocheza
Kitu kilichompa umaarufu Bruna ni ubora wake kwenye filamu. Kazi hiyo inampatia pesa na ndiyo maana aliona kitu cha kawaida tu kumtema staa mwenye pochi la nguvu na kisha akaendelea na maisha yake.
Baadhi ya filamu alizocheza mrembo huyo ambaye
zimempatia pesa nyingi na dili za matangazo ya kibiashara ni pamoja na
‘Sitio do Picapau Amarelo’, ‘Mulheres Apaixonadas’, ‘Xuxa Especial de
Natal’, ‘Negocio da China’, ‘Xuxa Abracadabra’ na ‘Xuxa e o Tesouro da
Cidade Perdida’.
Mapenzi si pesa, hicho ndicho unachoweza kusema baada ya mrembo huyo kuamua kumtema supastaa Neymar mwenye pesa za nguvu.
Mrembo huyo aliamua kufuta picha zote alizopiga na
Neymar katika mitandao ya kijamii jambo ambalo lilifichua wazi kwamba
mapenzi ya wawili hao yaliyodumu kwa mwaka mmoja hayapo tena.
Bruna, ambaye kwa sasa anatamba kwenye tamthilia
ya ‘Em Familia’ inayoonyeshwa katika kituo cha Globo, uvumi wa yeye
kuachana na Neymar ulizagaa tangu Desemba mwaka jana kabla ya kila mmoja
kusherehekea Mwaka Mpya kivyake.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!