Ric Wee, ambaye alisafiri umbali wa maili 6,544.8
kutoka Malaysia hadi England kwa mara ya kwanza akiwa na lengo la kwenda
kuitazama Everton ikicheza ‘laivu’. Alifunga safari hiyo baada ya
kuishabikia timu hiyo kwa miaka 30 akiwa huko.
Aliamini tukio hilo lingekuwa la aina ya kipekee
kwake akisafiri umbali huo kwenda kuitazama timu yake anayoishangillia
ikicheza tena kwenye uwanja wa nyumbani wa Goodison Park. Ingekuwa mara
yake ya kwanza kwa maisha yake kuitazama Everton ikicheza ‘laivu’ baada
ya miaka yote 30 kuishia kuitazama kupitia televisheni.
Ndoto za miaka 30 zakwama
Wee akiamini kwamba ndoto zake za kuitazama
Everton kwa macho yake moja kwa moja ikicheza inatimia, aliketi jukwaani
uwanjani Goodison Park akisubiri muda tu wa mechi ufike kwani aliwahi
zaidi kufika uwanjani hapo.
Katika kuwaonyesha mashabiki wenzake aliowaacha
Malaysia, Wee alipiga picha inayomwonyesha akiwa uwanjani hapo na kisha
kuituma kwenye mtandao wa kijamii.
Lakini, dakika chache baadaye tangu alipoketi
kwenye viti vya Goodison Park, polisi walifika hapo na kutangaza kwamba
mechi ya soka kati ya wenyeji Everton na Crystal Palace imeahirishwa kwa
sababu ya hali mbaya ya hewa ambapo upepo uliangusha majengo yaliyopo
karibu na uwanja huo hivyo kulikuwa na hatari kubwa ya hali ya
kiusalama.
Ujumbe wake kwenye Twitter
Kwa furaha kubwa, shabiki huyo aliandika ujumbe
wake kwenye Twitter saa moja kabla ya mechi hiyo na aliandika:
“Hatimaye, miaka 30 tangu ya kuishabikia Everton, nitaitazama EFC
ikicheza ‘laivu’ kwa mara ya kwanza.”
Lakini, dakika chache baadaye tangazo la mechi
kuahirishwa lilitolewa na jambo hilo lilimfanya Wee kuonekana kuwa na
hasira kwa sababu ya hewa imemtibulia nafasi yake ya kuitazama Everton,
timu yake kipenzi ikicheza yeye akiwamo uwanjani kuishuhudia.
Baadaye alikaza moyo na kujifariji baada ya kutuma ujumbe
mwingine kwenye Twitter unaomwonyesha akiwa na ratiba za mechi za
Everton pamoja na tiketi ya mechi, aliandika: “Kwa bahati mbaya Everton
vs Palace mechi imeahirishwa kwa sababu ya hali ya hewa kuwa mbaya.
Ndoto ya kuitazama EFC bado ipo palepale.”
Atembezwa vyumbani
Jambo la bahati kwake ni kwamba shabiki huyo wa
kutupwa wa Everton alitulizwa kiasi na Everton baada ya kutembezwa
kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya timu hiyo na kukutana na mastaa
wa kikosi hicho.
Kwenye vyumba hivyo, Wee alionekana akifurahia
jambo na kocha wa Everton, Roberto Martinez na beki wa kushoto, Leighton
Baines, ambaye pia alimpa jezi iliyosainiwa ikiwa ni zawadi ya kurudi
nayo kwao Malaysia.
Lakini, Wee hakuwa shabiki pekee wa Everton
aliyesafiri kwa umbali mrefu kwenda kutazama mechi hiyo kwa mara ya
kwanza na kisha ikaahirishwa.
Baadaye klabu ya mashabiki wa Everton waishio
Malaysia waliandika kwenye ukurasa wao wa Twitter: “Wamalaysia
wanaoishabikia Everton, Ridhwan Razak na Ric Wee, watakwenda kuitazama
timu hiyo ikicheza kwa mara ya kwanza.”
Ujumbe huo ulitumwa siku moja kabla ya mechi hiyo ambayo haikufanyika.
Wafanyiwa mapokezi mazuri
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Everton, Alan Myers,
alisema baada ya Wee kushindwa kutimiza ndoto zake za kuitazama ‘laivu’
kwa mara ya kwanza klabu yake ikiwa uwanjani, klabu imechukua jukumu la
kumtembeza maeneo mbalimbali ya uwanjani Goodison Park ili kujionea
miundombinu katika klabu hiyo.
Jambo hilo lilipangwa kufanyika juzi Alhamisi
asubuhi na jioni Wee alitarajiwa kupanda ndege na kurudi Malaysia. Baada
ya kupata fursa ya kukutana na wachezaji mastaa wa kikosi hicho na
kuona vitu mbalimbali vya kihistoria kwenye klabu hiyo, Wee alishukuru
kwa mapokezi aliyoyapata na kuushukuru uongozi wa klabu hiyo kwa
kuwathamini mashabiki wao.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!