YANAPOTAJWA majina yao; David Fairclough, Ole Gunnar Solskjaer,
Tore Andre Flo na hawa wa siku za hivi karibuni akina Edin Dzeko na
Javier Hernandez, kitu cha kwanza kinachokuja akilini ni kwamba hao ni
wakali wa kubadili matokeo ya mchezo wa soka wanaoanzia kwenye benchi.
Kwenye mchezo wa soka kuna lugha yake inayowatambulisha watu hawa ‘Super Sub’.
Wachezaji wanaoanzishwa benchi kwenye mechi kadhaa
na kisha kila wanapoingizwa husababisha matokeo ya mchezo kubadilika
kwa maana ya kufunga mabao au kutengeneza mabao hayo, nyota hawa
hutambulika kwa jina la ‘Super Sub’.
Kwenye Ligi Kuu England, klabu za Manchester City,
Swansea na West Bromwich Albion, zimewatumia sana wachezaji hao na
kuvuna mabao 12 ambayo yamewasaidia katika kupata matokeo bora kwenye
mechi zao.
Lakini, katika mikikimikiki ya ligi hiyo, kuna
timu ambayo imechemsha na kushindwa kupata hata bao moja licha ya
kufanya mabadiliko mengi zaidi ya wachezaji kuliko klabu nyingine zote
kwenye Ligi Kuu England.
Norwich City ambayo kocha wake, Chris Hughton,
amebadilisha wachezaji mara 63, lakini hakuna hata mmoja kati ya nyota
wake walioanzia benchi aliyeweza kufunga mabao au kusababisha bao
kufungwa.
Hadi kufikia sasa kwenye msimu huu, kwenye matokeo
ambayo timu yake imefungwa, Hughton alifanya mabadiliko 63 ya wachezaji
akiwa na imani ya kubadili matokeo, lakini hakufanikiwa.
Wachezaji walioanzishwa benchi na kisha kuingizwa
uwanjani ili wakabadili matokeo, lakini wakashindwa kufanya hivyo ni
pamoja na Robert Snodgrass, Wes Hoolahan, Johan Elmander, Jonny Howson,
Anthony Pilkington, Alexander Tettey, Ryan Bennett, Gary Hooper, Nathan
Redmond, Josh Murphy, Steven Whittaker, Ricky van Wolfswinkel, Luciano
Becchio na Leroy Fer.
Kwenye Ligi Kuu England wakati kwa sasa upinzani
zaidi ukiwa umeongezeka kwenye nafasi nne za juu, katikati na mkiani,
kuna timu zimefaidika na wachezaji wanaoanzia benchi kutokana na
kusababisha matokeo mazuri kila wanapoingizwa.
Kwenye Top Four
Manchester City inashika nafasi ya tatu kwenye
msimamo wa Ligi Kuu England na pointi zake 54, tatu nyuma ya vinara
Chelsea. Lakini kikosi hicho kinachonolewa na Manuel Pellegrini,
kimevuna mabao mengi zaidi yaliyotokana na wachezaji wake walioanzia
benchi.
Ndani ya 10 bora
Timu za katikati
Timu hiyo imefanya mabadiliko mara 70 na wachezaji wanane
walifunga mabao na wengine wanne walitengeneza nafasi za kufunga na
kufanya jumla ya mabao 12.
Chelsea na Arsenal zote zimevuna mabao manane
yaliyotokana na wachezaji walioanzia benchi, lakini vinara wanaonolewa
na Mreno Jose Mourinho wakifanya mabadiliko mara 78 dhidi ya mara 70 za
kikosi cha Mfaransa, Arsene Wenger.
Kwenye orodha hiyo, wachezaji sita wa Chelsea
walifunga mabao na wawili walipiga pasi za mabao, wakati kwa upande wa
Arsenal ni nusu kwa nusu, wanne walifunga na wengine wanne walitengeneza
nafasi za mabao.
Liverpool imefanya mabadiliko mara 58 na wachezaji
wawili walifunga na wawili walitengeneza nafasi za mabao jambo
lililowafanya kuvuna mabao manne kutokana na wachezaji hao walioanzia
kwenye benchi.
Kwa jumla mabao 32 yalifungwa kutokana na
wachezaji walioanzia benchi kwenye timu zilizopo ndani ya nne bora
kwenye Ligi Kuu England.
Ndani ya 10 bora
Mabingwa watetezi, Manchester United, wamenasa
kwenye nafasi ya saba kwenye msimamo. Kocha wao, David Moyes, amefanya
mabadiliko 68 ya wachezaji kwa maana ya kutaka wabadilishe matokeo,
lakini amefunga mabao sita tu.
Kwenye kundi hili, Swansea inaoongoza baada ya
kuvuna mabao 12 kwa kufanya mabadiliko mara 62, nyota wanne wakifunga na
wengine wanane walitengeneza nafasi.
Timu nyingine zilizovuna mabao mengi ya wachezaji
wa akiba kwenye kundi hili ni Tottenham yenye mabao matano baada ya
kubadili wachezaji 71, Newcastle mabao saba kutoka kwa wachezaji 70,
Southampton mabao sita kutoka kwa wachezaji 70 na Everton imepata mabao
manane kutoka kwa wachezaji 68.
Timu za katikati
West Ham imefanya mabadiliko 77 ya wachezaji na
kuvuna jumla ya mabao tisa kwenye kundi la timu zinazodaiwa kuwa na
ushindani mkubwa kutokana na kugoma kuporomoka kwenye eneo la kushuka
daraja.
Crystal Palace imepata mabao sita baada ya
kubadili wachezaji mara 73, wakati Stoke City imebadili wachezaji mara
66 na kuvuna mabao sita pia, huku Hull City ikipata mabao matatu tu
kutoka kwa wachezaji 72 iliyowabadilisha sawa na Aston Villa iliyopata
idadi kama hiyo ya mabao, lakini yenyewe ikifanya mabadiliko 63 ya
wachezaji walioanzia benchi.
Mabao yaliyofungwa
Ndiko kwenye vita kali zaidi. Fulham wikiendi iliyopita
iliigomea Manchester United kabla ya Jumatano iliyopita kufungwa dakika
za mwisho na Liverpool, shukrani kwa mkwaju wa penalti wa dakika za
majeruhi wa kiungo, Steven Gerrard.
Hadi kufikia sasa kwenye ligi hiyo, Fulham
imefanya mabadiliko 73 ya wachezaji walioanzia benchi na kupata mabao
matano, lakini West Brom ikivuna mabao mengi zaidi kwa kupata 12 kutoka
kwa wachezaji 76 iliyowabadilisha.
Timu nyingine kwenye fungu hilo ni Cardiff City
ambayo imepata mabao sita kwa wachezaji 74, sawa na Sunderland
iliyofunga mabao kama hayo baada ya kubadilisha wachezaji 70, huku
Norwich City ikitia fora kwa kushindwa kufunga mabao licha ya
kubadilisha wachezaji mara 63.
Mabao yaliyofungwa
Kwenye orodha ya mabao yote yaliyofungwa na
wachezaji walioanzia benchi kwenye Ligi Kuu England msimu huu, ni 132
kati ya mabao 690 yaliyofungwa kwenye ligi hiyo baada ya wastani wa
mechi 26 kwa timu, licha ya baadhi ya timu ikiwamo Manchester City yenye
mabao mengi zaidi ya kufunga, kuwa nyuma kwa mchezo mmoja.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!