SIO sisi tu wala Arsenal au Manchester City, lakini hata
Liverpool wana nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England
msimu huu. Hiyo ni kauli ya kocha wa Chelsea, Jose Mourinho, akipima
joto la ligi hiyo maarufu duniani.
Ushindi wa mabao 3-2 wa Liverpool dhidi ya Fulham
wa Jumatano usiku, unaiacha klabu hiyo ya Merseyside kuwa pointi nne tu
nyuma ya vinara Chelsea huku zikiwa zimesalia mechi 12 kabla ya ligi
hiyo kumalizika.
Wakati Chelsea, Arsenal na Manchester City zikiwa
zinakabiliwa na mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya pia, Liverpool imebakiwa
na michuano ya Kombe la FA tu na ukweli huo unamfanya Mourinho aamini
kuwa hii ni faida kubwa kwa Liverpool.
“Wakati ninaposema sisi sio watarajiwa wakubwa wa
ubingwa, kila mtu hapa anaanza kusema kuwa nimeanza tabia yangu ya
kuchezeana akili. Lakini hizo ni hisia zangu tu. Ligi hii inashangaza
sana. Ni ngumu kwa kila mmoja wetu,” alisema Mourinho.
“Kuna ambazo zina nafasi kubwa kuliko nyingine.
Kwa mfano, kuna Liverpool ambayo ina nafasi kubwa kwa sababu haichezi
katika Ligi ya Mabingwa. Kucheza katika Ligi ya Mabingwa kunatumia nguvu
nyingi na umakini kwa timu zilizopo.
“Nadhani itachekesha sana. Tulipoteza pointi mbili
na kupata moja dhidi ya West Brom na nadhani itakuwa kama hivi mpaka
mwishoni mwa msimu. Kila timu inahitaji pointi kwa sababu mbalimbali.
Wengine ili wasishuke daraja, wengine kwa ajili ya kucheza Ligi ya
Mabingwa, kwa hiyo pointi zitakuwa ngumu.”
Katika mechi mbili zilizopita, Chelsea imeambulia
pointi nne, wakati Manchester City na Arsenal zote zimeambulia pointi
moja kila moja na hivyo kufanya mpambano wa timu za juu kuwa mkali.
Kiungo ambaye pia ni nahodha wa Liverpool, Steven
Gerrard, alikiri kwamba wao wamekuwa wakiufukuzia ubingwa kimya kimya
ingawa ni mapema kusema lolote kuhusu taji hilo.
“Sisi tunaendelea kucheza na kujaribu kushinda
mechi nyingi kadiri tuwezavyo. Tuna faida kwa sababu hatuchezi michuano
ya Ulaya, tuna Ligi tu na michuano ya FA ndio ambayo tunaizingatia kwa
umakini,” alisema Gerrard ambaye penalti yake ya dakika za majeruhi
iliipatia Liverpool ushindi muhimu.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!