Serikali ya Kenya imelilalamikia vikali shirika la misaada la Marekani
USAid kuwa linafanya njama za kuzusha machafuko nchini Kenya. Francis
Kimemia, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Usalama wa Taifa ya Kenya
ameushutumu Wakala wa Kimataifa wa Ustawi wa serikali ya Marekani USAid
kuwa unatumia fedha zake kuchochea maandamano dhidi ya serikali ya
Jubilee na unadhamini harakati za siri za kuleta machafuko nchini Kenya.
Asasi hiyo ya serikali ya Marekani iliasisiwa mwaka 1961 na inajifanya
kutoa misaada ya kifedha na isiyo ya kijeshi kwa nchi zenye maendeleo
madogo duniani. Hata hivyo shirika hilo la serikali ya Marekani limekuwa
likituhumiwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na hivi sasa
serikali ya Kenya inaishutumu Marekani kuwa inatumia asasi yake hiyo
kufanya njama dhidi ya serikali ya Jubilee. Francis Kimemia ameongeza
kuwa, lengo la njama hizo za Marekani ni kusukuma pole pole malalamiko
ya watu ndani ya Bunge la Kenya ili kuwachochea wabunge wa Kenya
waifanyie uadui serikali ya nchi hiyo. Nchi ya Kenya ni maarufu kwa jina
la lango la kuingilia eneo la mashariki mwa Afrika na ni moja ya nchi
zenye ushirikiano mkubwa na Marekani katika masuala mbalimbali. Hata
hivyo baada ya kuchaguliwa serikali ya Jubilee ya Rais Uhuru Kenyatta na
makamu wake William Ruto huko Kenya, uhusiano wa Marekani na Kenya
umeshuhudia malumbano ya mara kwa mara huku Rais wa Marekani akionesha
wazi kuwa hakufurahia kuingia madarakani serikali ya Jubilee. Kesi
zinazowakabili Uhuru Kenyatta na William Ruto huko ICC zilidaiwa kuwa
ndizo sababu zilizoifanya Marekani isifurahie viongozi hao wawili
kuingia madarakani nchini Kenya. Hata hivyo baadhi ya weledi wa mambo
wanasema, kuna sababu nyingine zilizoifanya Marekani na hasa Rais Barack
Obama wa nchi hiyo kuchukizwa na chaguo la Wakenya katika uchaguzi mkuu
uliopita. Alaakullihaal, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa,
katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imekuwa ikikwepa kuingia moja
kwa moja katika masuala ya kisiasa na kijeshi ya nchi za Afrika ingawa
hata hivyo imeelekeza nguvu zake zaidi upande wa Somalia. Umuhimu wa
kijiografia wa Somalia huko Pembe ya Afrika umetajwa kuwa ndio
uliowafanya viongozi wa Marekani waipe uzito mkubwa nchi hiyo. Hivi sasa
serikali ya Kenya inaishutumu Marekani kuwa inafanya njama za kuleta
machafuko ndani ya Kenya, baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanaamini kuwa
kuna uwezekano hatua ya Marekani ya kujaribu kuleta machafuko huko
Kenya ni kuifanya serikali ya Nairobi ishughulishwe na masuala yake ya
ndani ya kuachana na suala la Somalia ambako imetuma wanajeshi wake
kupambana na wanamgambo wa ash Shabab na hivyo kupunguza washindani wa
Marekani katika kadhia ya Somalia. Tamko kali la Kamati ya Ushauri wa
Usalama wa Taifa ya Kenya dhidi ya Marekani limetolewa baada ya
wanaharakati wa asasi za kijamii kufanya maandamano mjini Nairobi.
Waandamanaji wameituhumu serikali ya Jubilee kuwa imejaa ufisadi na
ubadhirifu na imeshindwa kupambana na umaskini, ukosefu wa kazi na
ukosefu wa usalama nchini Kenya. Kwa upande wake serikali ya Kenya
inaishutumu Marekani kuwa ndiyo inayochochea machafuko dhidi ya serikali
na inasema kuwa, ina ushahidi wa kutosha unaothibitisha kwamba asasi ya
serikali ya Marekani ya USAid ndiyo inayochochea uasi dhidi ya serikali
ya Jubilee. Ni jambo lililo wazi kuwa kuingilia masuala ya ndani ya
nchi nyingine ni kinyume na sheria za kimataifa, tab'an Marekani ina
historia chafu ya kutojali sheria zozote zile mbele ya malengo yake ya
kibeberu.
Home »
siasa afrika
» TAARIFA KUTOKA KENYA ZASEMA KUWA SERIKALI YA KENYA YAISHTUMU SERIKALI YA MAREKANI KWA UCHOCHEZI NCHINI HUMO
TAARIFA KUTOKA KENYA ZASEMA KUWA SERIKALI YA KENYA YAISHTUMU SERIKALI YA MAREKANI KWA UCHOCHEZI NCHINI HUMO
Written By Unknown on Saturday, 15 February 2014 | Saturday, February 15, 2014
Labels:
siasa afrika
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!