JOSE Mourinho hatari sana. Utasema nini zaidi ya hicho baada ya
jana Jumatatu usiku kumzidi mbinu Manuel Pellegrini kwa kumpangia kikosi
kijanja na kuisambaratisha Manchester City kwao kwa bao 1-0 katika
mchezo wa Ligi Kuu England na hivyo kutibua rekodi ya wenyeji wao
uwanjani Etihad.
Bao la shuti kali la beki wa kulia, Mserbia
Branislav Ivanovic kwenye dakika 32 lilitosha kumtoa kimasomaso Mourinho
na kikosi chake cha Chelsea na hivyo kufanikiwa kuitambia Manchester
City katika mechi zote mbili ilizocheza na timu hiyo kwenye Ligi Kuu.
Kwenye mchezo huo, Chelsea iliyocheza kwa nidhamu
kubwa ilistahili kushinda baada ya kufanya mashambulizi ya nguvu kwenye
goli la Manchester City na kugongesha mwamba mara tatu kupitia kwa
Samuel Eto’o, Nemanja Matic na Gary Cahill.
Chelsea ilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda mabao
mengi kwenye mchezo huo kwa sababu walikuwa tishio muda wote, huku
kiungo wao Mbelgiji, Eden Hazard akicheza kwa kiwango cha juu sana.
Lakini, pongezi kubwa ni kwa Mourinho aliyeingia na kikosi cha kijanja
sana.
Kwenye mchezo huo, Mourinho alianza na straika
mmoja tu, Eto’o, lakini alichokuwa akikifanya staa huyo wa Cameroon ni
kuwakaba mabeki wa kati wa Manchester City na kuwanyima uhuru wa
kupandisha mipira mbele. Kwenye kiungo Manchester City ilimkosa kiungo
wake muhimu,
Mbrazili Fernandinho huku Mourinho akiwaandisha
wachezaji wawili wakabaji, David Luiz na Matic, ambao walikuwa na kazi
moja tu ya kutibua mipango ya wapinzani wao pamoja na kumvuruga Yaya
Toure.
Mreno Mourinho alitumia mbinu sana baada ya
kumtumia Ramires kama mkabaji wa kuanzia mbele akishrikiana na Eto’o
jambo lilimfanya Hazard kuwa huru na kupanga mashambulizi ya kikosi
hicho cha Chelsea.
Matokeo hayo yalikuwa ya kwanza kwa Manchester City kwenye mechi 61 wakicheza nyumbani bila ya kupata bao tangu Novemba 2010.
Jinsi bao lilivyofungwa
Pasi fupi ilitoka kwa Eto’o, ambaye alipiga nyuma
kwa Azpilicueta. Azpilicueta alituliza na kupiga pasi ndefu kwa Hazard,
aliyekuwa upande wa kushoto.
Mbelgiji huyo alikokota mpira kuingia nao kwenye
goli la Manchester City na kupiga pasi kwa Ramires, ambaye alimgongea
Ivanovic na yeye akampenyezea Hazard tena. Hazard safari hii alikuwa
upande wa kulia, alipiga krosi kwa Ramires kabla ya mpira kumfikia
Ivanovic aliyefumua shuti kali la chinichini lililomshinda kipa Joe Hart
na kutinga wavuni.
Kwa bao hilo limeifanya Chelsea kukusanya pointi
tatu muhimu na sasa awamefikisha pointi 53 sawa na Manchester City
wakiwa wamezidiwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.Kwa matokeo hayo, Arsenal sasa itaendelea kubaki kwenye kilele cha
msimamo wa ligi hiyo baada ya kujikusanyia pointi 55, mbili zaidi ya
timu zinazomfuatia na hivyo Arsene Wenger kuendelea na matumaini yake ya
kunyakua ubingwa msimu huu.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!