Kiungo wa Manchester United,Marouane Fellaini
amekuja juu na kusema kuwa David Moyes ambaye anakiongoza kikosi cha
mashetani wekundu hao kwa msimu wake wa kwanza,atakuwa na mafanikio sana
kwa siku za usoni.
Fellaini alimfuata Moyes akitokea Everton
katika kipindi cha majira ya joto lakini umekuwa msimu wao wa kwanza
mbaya sana kwa wote wawili kufuatia Man United kuhaha kuonyesha ubora
wake na wakiwa katika hatihati ya kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya
ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Raia huyo wa Belgium anasema kuwa mara zote
imekuwa ngumu kwa Man United kustahimili maisha bila ya Sir Alex
Ferguson ila akaonyesha kumuunga mkono Moyes.
Huku akisisitiza kuwa,”Unapaswa kumpa David Moyes muda wa
kutosha.Yupo imara sana.Na ndiyo sababu anaweza kupambana na
presha.Kumpa muda kutamfanya awe meneja bora sana kwa Manchester
United.”Fellaini akaongeza kuwa hana wasiwasi wowote kuhusu ubora wa Moyes wa kuweza kuirudisha klabu hiyo katika kiwango kizuri huku akionyesha matumaini kwa mashabiki kuendelea kumuunga mkono.
Pia akadai kuwa,”Kinachoifanya Ma United kuwa tofauti ni kuwa wanadumu na mameneja.”Unaweza kutazama maisha ya Sir Alex Ferguson na aliiongoza klabu kwa miaka 26.”
Akaendelea kusema”Man United wamekuwa na meneja mmoja kwa kipindi cha miaka 26,hivyo kufanya mabadiliko hayo sio kitu rahisi kwa mtu yeyote yule.Uongozi,mashabiki na kila mtu wanapaswa kumpa muda.”
Fellaini amekuwa chini ya Moyes tangu kusajiliwa kwake katika klabu ya Everton akitokea Standard Liege mwaka 2008,na amempongeza na kumsifia meneja huyo kwa vyote alivyomfanyia.
Huku akisisitiza kuwa kamwe hawezi kuzungumza kitu kibaya kuhusu meneja huyo kwani amekuwa mtu muhimu sana kwenye maisha yake ya soka na amejifunza vitu vingi kutoka kwa raia huyo wa Scotland.
Nyota huyo akakiri kuwa amecheza michezo mingi sana akiwa Everton na mara zote Moyes alikuwa akimwambia ukweli kuhusu kiwango chake bila ya kumficha iwapo atacheza vibaya ama vizuri na kumwambia aongezee juhudi zaidi na kujituma.
Fellaini akasisitiza tena kuwa kwa vitu vyote alivyofanyiwa na Moyes hana budi kumlipa fadhila katika klabu ya Manchester United kwasasa.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!