Mahakam ya Kimataifa ya Uhalifu
imeamrisha Serikali ya Kenya ishurutishe mashahidi wanane kufika mbele
ya mahakama hiyo kutoa ushahidi dhidi ya Naibu Rais William Ruto na
mwanahabari Joshua arap Sang.
Uamuzi huo
umetolewa kufuatia ombi la Kiongozi wa Mashtaka Fatou Bensouda, aliyedai
mashahidi hao walishawishiwa kwa njia tofauti, ikiwemo vitisho na kwa
kuhongwa, ili waache kushirikiana naye kwenye kesi hiyo.
Bi Fatou Bensouda |
“Mahakama ilipata kuwa
Serikali ya Kenya ina jukumu la kushirikiana kikamilifu na mahakama kwa
kukabidhi mashahidi amri ya kufika mahakamani na kusaidia katika
kuwashurutisha wafike mbele ya mahakama, kwa kutumia mbinu yoyote
iwezekanavyo kuwalazimisha,” uamuzi huo ulisema.
Kenya ina
wajibu pia wa kufanikisha kushiriki kwa mashahidi hao kupitia
kiunganishi cha video na pia kuwahakikishia usalama wao hadi wafike
mbele ya mahakama hiyo.
Mawakili wa wawili hao
walikuwa wamepinga ombi hilo na kutaka mahakama itoe tu ombi la kuwataka
wanane hao wafike mahakamani, bila kuwalazimisha.
Ombi
Kwa upande
wake, Serikali kupitia kwa Mkuu wa Sheria Profesa Githu Muigai ilikuwa
imejitetea kuwa ombi hilo la Bi Bensouda halingeweza kutekelezwa kwa
kuwa lingekiuka sheria za kitaifa.
Kulingana na Profesa Muigai, sheria zinahitaji mashahidi wafike mbele ya mahakama kwa hiari bila kulazimishwa na yeyote.
Hata hivyo,
mahakama ilisema kuwa uamuzi wao unaambatana na sheria za kimataifa
pamoja na Mkataba wa Roma unaounda sheria za ICC.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!