Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani anayeshughulikia masuala ya
usalama nchini Tunisia ameonya kutokana na hatari na vitendo vya
uharibifu vya kundi la Kisalafi la 'Answaru Sharia' kwa nchi hiyo na
nchi nyingine jirani.
Ridha Sifr amesisitiza kuwa, kundi la Answaru Sharia ambalo
linajiarifisha kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaida,
limejiandaa kutekeleza uharibifu nchini Tunisia na nchi nyingine jirani.
Amesema kuwa, moja ya matatizo makubwa yanayoikabili nchi yake hivi
sasa ni kupakana Tunisia na nchi zenye machafuko kama Libya ambako
makundi mengi yenye kufurutu ada yanaendesha harakati zao na kuingia
baadhi ya wanachama hao nchini Tunisia. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani
anayeshughulikia masuala ya usalama nchini Tunisia, amekiri kwamba
serikali imeshindwa kurejesha misikiti iliyoporwa na wanachama wa kundi
hilo na kusisitiza kuwa, hadi sasa misikiti 150 katika maeneo tofauti ya
nchi hiyo, haipo chini ya udhibiti wa serikali suala ambalo ni hatari
sana kwa taifa.
Itakumbukwa kuwa tarehe 27 mwezi Agosti mwaka jana, serikali ya Tunis
ililitangaza kundi hilo kuwa la kigaidi na kwamba ndilo lililotekeleza
mauaji dhidi ya wanasiasa wawili wa nchi hiyo ambao ni Chokri Belaid na
Mohammad Al Barahimi.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!