Headlines News :
USWAZI MAGAZINE
Home » » KAMPENI ZA UCHAGUZI WA RAIS ZAANZA NCHINI GUINEA BISSAU

KAMPENI ZA UCHAGUZI WA RAIS ZAANZA NCHINI GUINEA BISSAU

Written By Unknown on Monday, 5 May 2014 | Monday, May 05, 2014

Kampeni za uchaguzi wa Rais nchini Guinea-Bissau zilianza rasmi hapo jana huku kila mgombea akifungua kampeni zake kwa mbwembwe za aina yake. Wagombea wawili yaani Jose Mario Vaz Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo na Nuno Gomes Nabiam mgombea wa kujitegemea ndio watakaochuana katika duru hii ya pili ya uchaguzi huo baada ya kuongoza katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo uliofanyika tarehe 13 ya mwezi uliopita wa Aprili.  Uchaguzi huo unahesabiwa kuwa na umuhimu wa aina yake hasa kwa kutilia maanani kwamba, unafanyika miaka miwili baada ya mapinduzi ya kijeshi. Aidha uchaguzi huo unafanyika baada ya kumalizika kipindi cha mpito.
Baada ya kuundwa serikali ya mpito, mara kadhaa uchaguzi wa Bunge na Rais nchini Guinea-Bissau uliakhirishwa kutokana na kukosekana fedha za kuendeshea zoezi la uchaguzi huo. Desemba mwaka uliopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitishia serikali ya mpito ya Guinea-Bissau kwamba, kama haitaitisha uchaguzi basi itaiwekea vikwazo. Aidha wanachama wa Baraza la Usalama waliwaonya wale wote wanaopinga Guinea-Bissau kurejea katika mkondo wa utawala wa sheria. Ala kulli haal, Aprili 13 mwezi uliopita uchaguzi wa Rais ulifanyika ambapo wagombea wapatao wanane walivutiwa na kiti hicho cha Urais huku mamia ya wagombea wengine wakipigana vikumbo kuwania viti 102 vya Bunge la Guinea-Bissau.
Hata hivyo kati ya vyama 15 vilivyotaka kushiriki katika uchaguzi wa Bunge ni vyama saba tu vya kisiasa ndivyo vilivyopasishwa na Tume ya Uchaguzi baada ya kutimiza masharti. Katika hali ambayo Kumba Yala Rais wa zamani wa nchi hiyo alikuwa akitajwa kuwa miongoni mwa wagombea watajika ambaye angeshiriki katika uchaguzi huo, aliaga dunia wiki mbili kabla ya uchaguzi huo. Hivi sasa wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, Jose Mario Vaz mgombea wa chama cha African Party for the Independence of Guinea-Bissau ana nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika duru ya pili ya uchaguzi wa Rais uliopangwa kufanyika tarehe 18 ya mwezi huu. Katika mahojiano yake na vyombo vya habari, Jose Mario Vaz amesisitiza kwamba, endapo atashindwa na Nuno Gomes Nabiam katika kinyang'anyiro cha Urais, bado chama chake kitakuwa na nafasi ya kutoa Waziri Mkuu kwani kinaweza kunyakua akthari ya viti vya Bunge la nchi hiyo.
Baada ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa Guinea Bissau kufanyika kwa amani na utulivu, Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitoa wito wa kuondolewa vikwazo nchi hiyo ilivyowekewa miaka miwili iliyopita baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi. Ukosefu wa amani huko Guinea Bissau uliwafanya baadhi ya majenerali wa jeshi kushiriki katika magendo ya madawa ya kulevya na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa gati kuu ya mihadarati inayopelekwa barani Ulaya. Hivi sasa wataalamu wa mambo wana matumaini kwamba, duru ya pili ya uchaguzi wa Guinea Bissau itapelekea kupatikana Rais aliyechaguliwa na wananchi, ambaye atachukua hatua za kuhitimisha hali ya vurugu na mchafukoge katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Share Na Jamaa Yako :

0 comments:

Toa Maoni yako

Tuambie Unafikilia Nini..!

Followers

Facebook Fan Page

Tukutane Twitter

Walio Tembelea Website Hii

Advertise

Smiley face
 
Support : Ismail Niyonkuru | Gody Godwin Unstoppable
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Ahabona 24 - Haki Zote Zimehifadhiwa
Template Design by Gody Godwin Unstoppable Published by Uswazi