Mshambuliaji wa Simba mwenye asili ya Burundi anae julikana kwa jina la Amissi Tambwe,inasemekana ametua kwa siri jijini Dar
es Salaam na amefichwa akiwa chini ya ulinzi mkali kwa hofu kwamba
Yanga inaweza kumshawishi ili kumchomoa Msimbazi.
Lakini si hilo tu, kufichwa kwake huko kulikofanywa na
mmoja wa vigogo wanaowania urais wa Simba kwenye uchaguzi mwishoni mwa
mwezi huu, pia kunalenga kumweka mbali na wapinzani wake kwenye uchaguzi
huo akihisi wanaweza kumnasa, wakamrubuni na kumtumia kama sehemu ya
kampeni na kumzidi kete.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zinadai
kwamba baadhi ya vichwa vya kamati ya usajili vimefanya mazungumzo ya
siri sana na mchezaji huyo wakiangalia uwezekano wa kusitisha mkataba
wake wa mwaka mmoja aliobakiza kwenye club ya Simba.
Inadaiwa kwamba Yanga walikuwa wakimshawishi
mchezaji huyo atumie sababu kuwa amepata timu nje na watakachofanya wao
ni kumwongezea dau la usajili na mshahara zaidi ya mara mbili ya ule wa
dola 800 anaopokea Simba. Lakini Simba wameshtukia dili na sasa wamekaba
kila kona.
Wamehakikisha kwamba katika muda ambao Tambwe
atakuwa Dar es Salaam hazururi ovyo na hapati upenyo wa kuzungumza na
watu wa Yanga na hata simu yake haipatikani muda wote.
Tambwe alisema alikiri kwamba yupo Dar es Salaam, lakini hataki kuzungumzia
mambo ya mpira kwa sasa kwa vile yanamweka kwenye wakati mgumu.
“Yananiweka kwenye wakati mgumu sana, labda nitafute kesho ndugu yangu,”alisema Tambwe kwa kifupi.
Siri imeanza kufichuka kuwa Tambwe yupo kwenye hoteli moja maeneo ya Ubungo lakini hataki yeyote ajue zaidi waliomleta.
Taarifa za uhakika ambazo mtandao huu umezipata
kutoka kwa mtu wa karibu wa mshambuliaji huyo, zimeeleza kuwa Tambwe
alitua nchini Tanzania mapema wiki hii akitokea nchini Burundi, lakini ujio huo
ukifanywa siri kubwa ikiwa ni pamoja na kubadilishiwa sehemu ya kuishi.
Habari za ndani ya Simba zinasema sababu kubwa ya
kumleta Tambwe Tanzania kabla ya muda wa kurudi kujiunga na timu hiyo ni
kuweka sawa masuala yake ya mkataba na mambo madogo madogo yaliyokuwa
na utata. Pia kumkabidhi tuzo yake aliyopatiwa na wadhamini wa Ligi Kuu,
Kampuni ya Vodacom sambamba na Sh5.2milioni za kuwa Mfungaji Bora.
Alipo tafutwa Katibu Mkuu wa Simba,
Ezekiel Kamwaga, ambaye alikiri uwepo wa Tambwe nchini Tanzania akisema amekuja
kuchukua kiasi cha fedha alichopatiwa na mtandao wa simu wa Vodacom huku akigoma kueleza
sababu ya kufichwa kwa safari hiyo na hata kumhamisha alipokuwa anaishi.
“Nani amekwambia hizo taarifa? Kweli Tambwe yuko
nchini, uongozi ndio uliomleta. Kama unavyojua, tupo katika uchaguzi
lakini sekretarieti ipo na inafanya kazi zake. Amekuja kuchukua zawadi
yake ya ufungaji bora sambamba na kuchukua fedha zake, mengine siwezi
kukueleza,” alisema Kamwaga na kukata simu.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!