Ingekuwa kwa Burundi, fungu la pauni milioni 100 (zaidi ya Sh
bilioni 260) zimetengwa kwa ajili ya kusajili wachezaji ili kuimarisha kikosi,
basi kocha angechanganyikiwa.
Lakini kwa Arsene Wenger wa Arsenal, bado atalazimika kuwa makini sana
ili kupata anachotaka kwa kuwa angalau asajili wachezaji sita, mabeki, viungo
na washambuliaji.
Wachezaji 10 wafuatao ndiyo sehemu sahihi Wenger anaweza kuchagua
ili alitumie dau lake la pauni milioni 100 ambazo uongozi wa Arsenal umempa
baada ya kubeba ubingwa wa Kombe la FA.
Baada ya ubingwa huo, Wenger amefukia njaa ya makombe Arsenal ambayo
ilikaukiwa kupitiliza. Sasa ni kazi ya kuusaka ubingwa wa England na akiwapata
angalau watano kati ya hawa 10, Arsenal itatisha 2014-15.
Calum Chambers (Southampton) |
Amecheza mechi 22 katika Premiership na ndiyo ana miaka 19 na uwezo
wake umekuwa juu hadi kufikia kumshawishi Kocha Mkuu wa England, Roy Hodgson
kumuweka kwenye majina ya akiba.
Amepiga krosi 87 kwa msimu mzima ambazo ni asilimia 87 za ubora kwa
krosi.
Atsuto Uchida (Schalke) |
Uchida ni raia wa Japan ambaye amefanya vizuri sana akiwa na Schalke. Mara baada ya kuondoka Japan akiwa na Kashima Antlers, Uchida amekuwa mchezaji bora zaidi kwa kikosi hicho kinachoshiriki Bundesliga.
Amecheza mechi 127 akiwa na Schalke, pia ameichezea Japan mechi 67.
Serge Aurier (Toulouse) |
Ana miaka 21 tu na aliwahi kumueleza Wenger kuwa kama atampa ofa,
yuko tayari kuondoka Ufaransa.
Lars Bender (Bayer Leverkusen) |
Nusura Wenger amtwae Bender msimu uliopita, lakini alipoambiwa kuna
uwezekano wa kumpata Mathieu Flamini akaona ni bora kufanya hivyo.
Kiungo huyo ana nguvu na ataifanya Arsenal ianze kutembea tangu
kwenye kiungo, kwani haina mtu wa uhakika kwenye nafasi hiyo.
Leverkusen walisema wanahitaji pauni milioni 20, lakini inaweza
ikawa imeongezeka kutokana na uwezo aliouonyesha.
Morgan Schneiderlin (Southampton) |
Schneiderlin amefanikiwa kutwaa tuzo mbili za mchezaji bora wa mwaka
aliyechaguliwa na wachezaji na ile ya aliyechaguliwa na mashabiki.
Kasi ya kiungo cha Arsenal ni tatizo, Arteta anazidi kupungua kasi
kutokana na umri. Schneiderlin raia wa Ufaransa ndiyo kwanza anaanza, anapiga
mashuti, anakaba na anachezesha timu hasa.
Amevuruga muvu 139, ameokoa mipira 146 kwa kulala na pasi bora za
uchezeshaji na ubora wake kwenye Premiership ni asilimia 84.
Cesc Fabregas (Barcelona) |
Hata kama itasajili viungo wawili, huu ndiyo wakati wa Fabregas
kurudi Arsenal, lakini ikishindikana Schneiderlin atakuwa msaada mkubwa.
Nafasi ya Fabregas inaonekana ipo kwa kuwa uwezo wake, aina ya
mifumo ya Arsenal aliizoea, utaona hata baada ya kuondoka, kikosi kikayumba.
Dau la pauni milioni 30 linaweza kuwa tatizo kwa Arsenal kwa kuwa
inahitaji kupata wachezaji wengi. Mabao 19 aliyofunga kwenye La Liga
yanaonyesha bado ni mzima na Wenger anaweza kumtumia kama namba 10 na akafanya
vizuri zaidi.
Alvaro Morata (Real Madrid) |
Tayari bosi wa Arsenal ameishafikisha ombi lake kwa Real Madrid
kwamba wanamtaka Morata, 21.
Huu ndiyo wakati mwafaka wa Wenger kumpata Morata na kama humjui,
angalia mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati Madrid ikiivaa
Atletico pale alipoingia kuchukua nafasi ya Karim Benzema.
Morata amecheza mechi 23 za La Liga, maana yake msimu ujao ana
nafasi ya kucheza zaidi.
Arsenal inahitaji mfungaji sahihi, msimu uliopita ilifunga mabao 68,
angalia mabingwa Man City wamefunga 102, Liverpool 101. Kuna tatizo pale.
Karim Benzema (Real Madrid) |
Kati ya Benzema au Morata, mmoja wao ana nafasi ya kuimarisha
kikosi, Benzema ana uwezo mkubwa wa kufunga, mabao yake 24 huku akitengeneza 16
ni jibu kuwa yuko sawasawa na atakuwa msaada Emirates kwa kuwa ana uhakika wa
kufunga mabao kuanzia 20 kwa msimu.
Mario Mandzukic (Bayern Munich) |
Mkali Robert Lewandowski atatua Bayern akitokea Borussia Dortmund,
hivyo ni rahisi kwa Arsenal kumpata Mandzukic mwenye ‘urafiki’ na nyavu.
Mandzukic pia amekuwa akiwaniwa na Manchester United na Chelsea,
lakini kama Arsenal itakuwa na mtu kama yeye, halafu acheze na Benzema au
Morata, itakuwa shughuli.
Inaonyesha ana uhakika wa kufunga hadi mabao 25 kwa msimu, amemaliza
msimu akiwa na mabao 26. Hata Bayern inaonekana kutokuwa na uhakika wa kumuuza,
ila uhusiano wake na Kocha Pep Guardola, umeyumba.
Loic Remy (Queens Park Rangers) |
Kocha mkongwe England, Harry Redknapp anaijua kazi ya Remy, ingawa
ameipandisha QPR kurejea Premiership, lakini kutompata Remy kunaonyesha
kuanzisha matatizo kwake.
Amefunga mabao 14 katika mechi 26 na amekuwa chachu ya ushindi na
anafananishwa na Nicholas Anelka wakati akiwa Arsenal na Wenger anaweza
kumtumia kama kiungo wa pembeni ambaye atakuwa anaingia ndani kumaliza kazi.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!