Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetahadharisha katika ripoti yake juu ya kuongezeka utumikishwaji wa watoto vitani huko Sudan Kusini. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwenendo wa watoto wanaotumiwa kama askari vitani umeongezeka katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya vikosi vya serikali ya Juba na waasi wanaoongozwa na Riek Machar aliyewahi kuwa Makamu wa Rais. Shirika la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Sudan Kusini kuwarejesha katika familia zao watoto wote ambao wanatumiwa na jeshi la serikali kama askari vitani. Kuwatumia watoto vitani kama askari ni jambo lisilofaa kwa mujibu wa sheria za Sudan Kusini na hata sheria za kimataifa.
Machafuko ya Sudan Kusini ambayo yalianza Disemba mwaka jana, hadi sasa yamesababisha maelfu ya watu kuuawa. Aidha zaidi ya watu milioni moja na nusu wamekuwa wakimbizi kufuatia mapigano hayo. Suala la kuwatumia watoto kama askari vitani linalofanywa na jeshi na waasi haliishii katika nchi ya Sudan Kusini pekee; suala hilo limeenea katika nchi nyingi ambazo zinakabaliwa na machafuko barani Afrika. Mbali na Sudan Kusini, kuna nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Somalia, Zimbabwe, Sudan na Uganda ambazo suala la kuwafanya watoto askari ni jambo la kawaida na lililoenea baina ya waasi na vikosi vya majeshi ya serikali. Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waasi wanaofungamana na makundi mbalimbali wamekuwa wakishambulia miji na vijiji tofauti vya nchi hiyo ambapo baada ya kuwateka nyara watoto, baadaye huwatumikisha watoto hao kama wapiganaji. Watoto hao mbali na kufanywa askari, hutumiwa pia katika masuala mbalimbali kama ya ulinzi, ujasusi, utumwa na propaganda vitani. Nchini Burundi pia kuna mamia ya watoto katika makundi ya waasi yanayojihusisha na harakati za kijeshi. Aidha inaelezwa kwamba, watoto wamekuwa wakitumiwa pia katika jeshi la Burundi. Kuenea utumiwaji vibaya watoto barani Afrika kunaendelea kufanyika katika hali ambayo, kuna mikataba mbalimbali iliyopasishwa kwa ajili ya kuzuia watoto kushiriki katika vita. Kwa mujibu wa kipengee namba 38 cha Mkataba wa Haki za Watoto, makundi ya kisiasa hayapaswi kuwatumia vitani watu wenye umri wa chini ya miaka 15. Aidha kwa mujibu wa Protokali ya Hiari ya Kushiriki Watoto Vitani, pande zinazopigana zinatakiwa kutowaruhusu kushiriki katika vita watu walio na umri wa chini ya miaka 18 na kwamba, kuwachukua kwa nguvu watu hao na kuwafanya askari ni jambo lililopigwa marufuku. Madola ya Magharibi yanaonesha kusikitishwa na vitendo vya kuongezeka utumiaji watoto kama askari barani Afrika. Hata hivyo hatua ya viongozi wa Magharibi ya kulaani utumiaji mabavu na kutumiwa watoto vitani inatathminiwa na wajuzi wa mambo kwamba, kwa nia ya kipropaganda, lengo likiwa ni kuzihadaa fikra za walio wengi ulimwenguni. Mashirika ya kigeni barani Afrika yamekuwa yakiunga mkono kuendelea machafuko katika nchi za bara hilo na hata yenyewe yanatajwa kuwa chanzo halisi cha machafuko hayo.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!