Shirika la Afya Duniani (WHO)
limetangaza kuwa idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na maradhi
hatari ya Ebola katika nchi nne za magharibi mwa Afrika imefikia 1229.
WHO limesema kuwa idadi hiyo ya vifo imeongezeka kati ya Agosti 14 hadi
16 mwaka huu, muda ambao ulisajili kesi mpya 113 za Ebola. Jumuiya ya
Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) imesema kuwa mripuko wa homa ya ebola
unaenea kwa kasi kuliko vile serikali zinavyoweza kukabiliana na maradhi
hayo na kwamba itachukua muda wa miezi sita kuudhibiti ugonjwa huo.
Shirika la Afya Duniani juzi lilizitaka
nchi zilizoathiriwa na maambukizo ya homa hatari ya Ebola kuwachunguza
wasafiri wote katika viwanja vya ndege, bandari na vivuko vya nchi kavu
wanaosafiri nje ya nchi. Hadi sasa hakuna tiba ya ugonjwa wa Ebola,
homa ambayo huambatana na dalili za mtu kuhara, kutapika na kutokwa na
damu. Guinea, Liberia na Sierra Leone zimeathiriwa vibaya na homa ya
Ebola ambayo sasa hivi pia imeingia huko Nigeria.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!